Mitego ya Shetani مكائد الشيطان

6.00 MB 40 1 Files
albyan
or download free
[free_download_btn]

Description

"Hakika Shetani ni adui yenu, basi mchukulieni kama adui..." [Qur'an 35:6]
Jifunza dini yako
Mtu mwenye busara ni yule anayechunguza mikakati ya adui zake na kuchukua tahadhari ili kuwashinda. Mola wako amekuhadharisha aliposema, “Hakika Shetani ni adui yenu, basi mchukulieni kama adui...” [Qur'an 35:6]
Historia ya Shetani (Iblis)
Shetani aliumbwa kutokana na moto usio na moshi. Ingawa hakuwa malaika, alikuwepo kati yao Peponi kutokana na utiifu wake kwa Allah. Allah alipomuumba Nabii Adam (amani iwe juu yake), Aliwaamuru waliokuwa Peponi kumsujudia Adam, lakini Shetani alikataa kwa kiburi na majivuno, akisema: "Mimi ni bora kuliko yeye [Adam]. Umeniumba kutokana na moto, naye umemuumba kutokana na udongo." [Qur’an 7:12]
Allah alimlaani Shetani na kumfukuza kutoka Peponi. Shetani akaomba nafasi ya kupotosha wanadamu, na Allah akampa ombi lake.
"[Shetani] alisema, ‘Kwa kuwa Umenipoteza, nitawakalia njiani kwenye njia yako iliyonyooka." "Kisha nitawajia  kutoka mbele yao, nyuma yao, kulia kwao, na kushoto kwao, na hutawakuta wengi wao wakishukuru." [Qur’an 7:16-17]
Mitego ya Shetani
Kukataa Upweke wa Allah
Msingi wa Uislamu ni kuamini Upweke wa Allah - bila mshirika, mfano, mwana au mpinzani. Kinyume chake, dhambi kubwa zaidi ni kumshirikisha Allah au kumfanya sawa na chochote.
Mifano ni pamoja na:

·        Kuielekeza ibada kwa asiyekuwa Allah (mfano: kusujudia au kuomba kwa asiyekuwa Allah).

·        Kuhusisha baadhi ya sifa za Allah kwa vitu au viumbe wengine (mfano: sanamu/vito vya mafundo ).

·        Kudai kwamba Allah ana mwana, mama au mshirika mwingine.

Kwa hivyo, kuwapotosha wanadamu kuelekea ukafiri ni lengo kuu la Shetani.

Hata hivyo, kama Shetani hawezi kuwapotosha watu kutenda vitendo vya wazi vya ukafiri,

Anakimbilia njia za siri zaidi, kama vile kuamini ushirikina, hirizi, unajimu na utabiri wa nyota. Imani kama hizi zinapingana na ukweli kwamba Allah pekee ndiye mwenye nguvu na ujuzi juu ya kila kitu, na Yeye pekee ndiye Anayeweza kuleta manufaa au madhara.

Uzushi katika Dini
"...Leo nimekukamilishieni dini yenu..." [Qur'an 5:3]
Shetani atamshawishi mtu kubuni imani na vitendo vibaya katika Uislamu ambavyo havikuamrishwa na Allah wala Mtume Muhammad (rehma na amani zimshukie). Kwa hakika, kuamini kuwa Uislamu haujakamilika au haujafunuliwa kikamilifu na Allah, hivyo unahitaji uzushi, kunachukuliwa kuwa ni ukafiri; kwa sababu ni kukataa yale aliyofunua Allah.
Uzushi mwingi hutekelezwa kwa uangalifu mkubwa kama kwamba ni ibada ya kidini, na huchukuliwa kuwa sawa na yale aliyofunua Allah. Hatari iko hapa, kwani watu wanaofuata uzushi huamini matendo yao yanakubaliwa, ingawa kwa hakika wanafanya dhambi. Wazushi hawa hawataona haja ya kutubu, kwa sababu hawatambui makosa yao.
 Kutotekeleza vizuri Matendo ya Lazima
"Hakika Swala inakataza machafu na maovu..." [Qur'an 29:45]
"Na Shetani anataka kuwazuieeni katika kumkumbuka Allah na swala..." [Qur'an 5:91]
Allah ameifanya baadhi ya matendo kuwa ya lazima kwa kila Muislamu, na linalofanyika mara kwa mara zaidi ni swala tano za kila siku. Kwa hivyo, Shetani anajaribu kutufanya tuipuuze swala ili tuanguke zaidi katika madhambi.
Udanganyifu wa kiPolepole
Mtume Muhammad (rehma na amani zimshukie) alitueleza jinsi ibada ya masanamu ilivyoanza, ikionyesha mbinu ya Shetani ya taratibu na uvumilivu. Baada ya kundi la watu wema kufariki, Shetani aliwahamasisha waliokuwa karibu nao kusimamisha sanamu kwa heshima yao na kama ukumbusho wa wema wao. Wakati kizazi kile kilipopita na watu wakasahau sababu ya kusimamishwa kwa sanamu hizo, Shetani aliwadanganya kuwaamini kwamba mababu zao walikuwa wakiabudu sanamu hizo, na kwamba kupitia hizo, mvua ililetwa. Kisha watu walianza kuabudu sanamu hizo.
Udanganyifu huu wa kipolepole hutumika kwa njia nyingi. Kwa mfano, Shetani huwadanganya watu kutenda matendo ya zinaa: huanza na jicho, kisha mawazo, tabasamu, mazungumzo yasiyo na hatia, kutengwa, na hatimaye dhambi yenyewe.
Vivyo hivyo, katika kutaka kuwafanya watu waache matendo yao ya lazima ya kidini,

Shetani huwashawishi watu mwanzoni kuacha ibada za hiari, ambayo huwpeleka kuwa wavivu na ibada za lazima. Pia anajaribu kuzipuuza dhambi ndogo, ambayo mwishowe huwaongoza kutumbukia kwenye madhambi makubwa.

Kupamba Matendo Maovu
"... Na Shetani akawapambia yale waliyokuwa wakiyatenda." [Qur'an 6:43]
Shetani huwafanya watu waone dhambi kwa sura ya kuvutia, kama alivyomdanganya Adam na Hawa kula kutoka kwenye mti.
Shetani alimnong'oneza Adam, akisema,

"Ewe Adam! Nikuelekeze kwenye Mti wa Umilele na ufalme usioharibika?" [Qur'an 20:120]

"Mola wenu hakuwakatazeni huu mti isipokuwa ili msije mkawa malaika au mkaingia kwenye umilele..." "Na hakika mimi ni mshauri wa kweli kwenu." "Basi akawadanganya kwa udanganyifu." "Na walipoonja yale matunda ya mti tupu zao zilifichuka… Mola wao akawaita." "Je, Sikuwaambia msile matunda ya mti huo, na Sikuwaambia kwamba Shetani ni adui yenu wa wazi?" [Qur'an 7:20-22]
Ingawa Adam alikuwa amezungukwa na vyakula vingi vilivyohalalishwa, Shetani alimshawishi kula kutoka kwenye mti ulioharamishwa. Vivyo hivyo, Shetani huwadanganya watu kufanya vitendo vilivyokatazwa badala ya vile vilivyoruhusiwa, kama vile uzinzi badala ya ndoa, muziki badala ya Qur'an, mapato haramu badala ya halali,

na kiwango kidogo cha vyakula na vinywaji vilivyokatazwa  kula badala ya vile vingi vilivyo safi na vyema.

Kuchochea matamanio
"Shetani huwaahidi na kuwachochea matamanio zao, lakini Shetani hawaahidi isipokuwa udanganyifu." [Qur'an 4:120]
Kila mwanadamu ana matamanio na vishawishi. Shetani hutumia hii na kumshawishi mwanadamu kujihusisha na starehe za haraka bila kufikiria matokeo. Hili hupelekea majuto na udhalili, aidha katika maisha haya au Siku ya Kiyama.
Kupoteza Muda
Kama Shetani hawezi kumtega mtu kufanya madhambi, humshughulisha na mambo yasiyo na manufaa yoyote. Badala ya kutumia muda wetu kwa busara, kutimiza vipaumbele vyetu na kufanikisha malengo ya juu, Shetani hutushughulisha na mambo yasiyo na faida yoyote.
Jinsi ya Kumshinda Shetani
"Hakika Shetani ni adui yenu; basi mchukulieni kama ni adui..." [Qur'an 35:6]
Hatua ya kwanza ni kumtambua Shetani kama adui wetu: ukimjua adui yako, unaweza kumshinda. Nguvu ya Shetani inatokana zaidi na uwezo wake wa kudanganya, kwa hivyo tunahitaji kuelewa mbinu zake za ujanja na mtazamo wake ili tuweze kujilinda vizuri zaidi.
Tafuta Msaada kwa Allah
Kuomba ulinzi kwa Allah na kumtegemea Yeye pekee kwa msaada ni silaha ya kumshinda Shetani. Surah Al-Falaq na An-Nas za Qur'an zinaweza kusomwa mara kwa mara ili kuomba ulinzi dhidi ya Shetani. Tunapaswa kutambua kwamba madamu tuko hai, Shetani hatakoma kamwe kujaribu kutupotosha. Lazima tuwe macho kila wakati na daima tumuombe Allah uongozi na ulinzi.
Omba  Msamaha

 

Mtume (rehma na amani zimshukie) alisema:
"Yeyote anayejutia madhambi ni kama mtu asiye na madhambi."
(Ibn Majah)
Iwapo tutashindwa na hila za Shetani, kwa neema na rehema za Allah bado tuna nafasi ya kujirekebisha makosa yetu kwa kukubali makosa yetu na kutubu kwa Allah.
Mtume (rehma na amani zimshukie) alisema:
"Shetani alimwambia Mwenyezi mungu  wa Utukufu, ‘Kwa Utukufu Wako, Ewe Mola, nitajaribu kuwatoa kwenye njia sahihi waja Wako maadamu roho zao zipo ndani ya miili yao.’ Mola akasema, ‘Kwa Utukufu Wangu na Ukuu Wangu, nitaendelea kuwasamehe maadamu wataomba msamaha Wangu.’"
(Ahmad)
Ili toba ikubalike, ni lazima iwe ya kweli, pamoja na nia ya kutorudia kwenye madhambi hiyo tena.
kuepuka Mazingira yenye madhambi
Usile katika hizi Wakati Allah alimkataza Adam dhidi ya mti mmoja, Hakusema: "Usile kutoka mti huu" bali alisema: "Wala msikaribie huu mti." [Qur'an 2:35] Kwa hivyo lazima tujiepushe na chochote kinachoweza kutupelekea kufanya dhambi.
Shikamana na Marafiki Wema
Mtu yuko katika dini ya rafiki yake wa karibu Mtume wa Allah (rehma na amani zimshukie) alitunasihi: ", basi angalieni ni nani mnayemfanya rafiki." [Tirmidhi]
Marafiki unaoshikamana nao wanaathiri sana maamuzi na matendo yako. Marafiki wema watakukumbusha kuhusu Allah na kukuhimiza kutenda mema, lakini marafiki wabaya watakuongoza mikononi mwa Shetani.
Fanya Matendo Mema
Kujishughulisha na matendo ya kidini, hasa swala, ni njia bora ya kumshinda Shetani. Ikiwa mtu atajishughulisha na mambo mema, kuna uwezekano mdogo wa kuathiriwa na hila za Shetani.
"Na kama shari yoyote itakujia kutoka kwa Shetani, basi omba ulinzi kutoka kwa  Allah. Hakika Yeye ni mwenye masikio na Mjuzi." [Qur'an 7:200]
Hitimisho
Vita dhidi ya Shetani vinaweza kushindwa tu ikiwa tunajua hila zake na kutumia mbinu za kumshinda. Siku ya Kiyama, Shetani atakiri dhambi zake na ufisadi wake. Atatangaza mbele ya viumbe wote kwamba Allah ndiye anayesema ukweli na kwamba yeye (Shetani) ni mwongo.
Tunamuomba Allah Mtukufu, kwa Majina Yake mazuri na Sifa Zake tukufu, atusamehe dhambi zetu na atulinde kutokana na hila za Shetani.

Similar Downloads

No related download found!