Description
Ufunuo wa Mwisho kwa wanadamu
Qur’ani Tukufu ni nini?
Maneno ya Mwenyezi Mungu
Qur’ani Tukufu ni maneeno halisi ya Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na aliye juu, aliloteremsha kwa Mtume Muhammad (rehma na amani zimshukie) kupitia Malaika Jibril.
"Kuteremshwa kwa Kitabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye Nguvu, Mwenye Hekima." (Qur'ani 39:1)
Mwongozo kwa wanadamu
Qur’ani Tukufu ni "Mwongozo kwa wanadamu... na kipimo cha kutofautisha (kati ya haki na batili)." (Qur'ani 2:185)
Inatoa mwongozo wa kusaidia wanadamu kutenganisha kati ya haki na batili, bila hiyo, mwanadamu bila shaka atapotea.
Ufunuo wa Mwisho
Qur’ani Tukufu ni Kitabu cha mwisho cha mbinguni kilichoteremshiwa na Mwenyezi Mungu, kinathibitisha ukweli kilichosalia katika baadhi ya maandiko ya awali na kukataa na kurekebisha upotoshaji na maongezi zilizomo katika matoleo ya sasa ya vitabu hivyo.
"Enyi watu wa Kitabu! Aminini yale tuliyoteremsha yanayothibitisha yale mliyo nayo..." (Qur'ani 4:47)
Qur’ani Tukufu iliteremshwa vipi?
Qur’ani Tukufu iliteremshwa kwa Mtume Muhammad (rehma na amani zimshukie) na ipo tu kwa lugha ambayo iliteremshwa - Kiarabu. Hata hivyo, tafsiri ya maana ya Qur’ani inapatikana kwa lugha mbalimbalii.
Qur’ani Tukufu haikuteremshwa kama kitabu kamili kwa mara moja; badala yake, ufunuo ulienea kwa kipindi cha miaka 23.
Kwa sababu hii, ni muhimu kujua mazingira ambayo aya ziliteremshwa ili kupata ufahamu sahihi wa Qur’ani; la sivyo, mafundisho yake yanaweza kueleweka vibaya.
Ninajuaje kama imetoka kwa Mwenyezi Mungu?
Ulinzi
Qur’ani Tukufu ndicho kitabu pekee cha kidini kilichosalia kuenea kwa muda mrefu na bado ni safi kama siku ilipoteremshwa. Hakuna kilichoongezwa, kuondolewa, au kubadilishwa tangu ilipoteremshwa zaidi ya miaka 1400 iliyopita.
"Hakika Sisi ndio tulioteremsha Qur, na hakika Sisi ni wenye kuilinda." (Qur’ani 15:9)
Qur’ani Tukufu haikuhifadhiwa tu kwa maandishi, bali pia katika nyoyo za wanaume, watoto, na wanawake. Leo, mamilioni ya watu wamehifadhi Qur’ani yote.
Miujiza ya Kisayansi
Qur’ani Tukufu haipingani na sayansi ya kisasa bali inaiunga mkono.
Moja ya mambo ya kushangaza kuhusu Qur’ani ni kwamba ina aya nyingi zinazoeleza kwa kina matukio ya kiasili katika nyanja mbalimbali kama vile embryolojia, hali ya hewa, astronomia, jiolojia na sayansi ya bahari.
Wanasayansi wamegundua kwamba maelezo yake ni sahihi kupita maelezo kwa kitabu hiki kilichotermshwa katika karne ya 7.
"Tutawaonyesha Ishara Zetu katika Ulimwengu na ndani ya nafsi zao wenyewe mpaka iwadhihirikie kwamba huu ni Ukweli." (Qur’ani 41:53)
Kwa hakika, miujiza mingi ya kisayansi iliyoelezwa katika Qur’ani imegunduliwa hivi karibuni tu kupitia maendeleo ya kisasa ya vifaa vya kiteknolojia.
Fikiria yafuatavyo:
· Qur’ani inatoa maelezo ya kina kuhusu maendeleo ya kiinitete cha binadamu. Maelezo haya hayakujulikana kwa jamii ya kisayansi hadi nyakati za hivi karibuni.
· Qur’ani inasema kuwa vyombo vya angani (nyota, sayari, miezi, nk...) vilitengenezwa kutoka kwa mawingu ya vumbi. Hapo awali haikujulikana, lakini sasa ni kanuni isiyopingikakatika elimu ya kozmolojia ya kisasa.
· Sayansi ya kisasa imegundua uwepo wa vizuizi vinavyoruhusu bahari mbili kukutana lakini kila moja ikibaki na halijoto, uzito na chumvi zake.
Ishara hizi za Mwenyezi Mungu zilielezwa wazi katika Qur’ani kabla ya miaka 1400 iliyopita.
Upekee
Tangu ilivyofunuliwa, hakuna mtu aliyewahi kuunda sura moja inayofanana na Qur’ani kwa uzuri wake, ufasaha, uzuri wa hekima yake, utaabiri na sifa zake nyinginezo za ukamilifu.
"Na kama mko katika shaka juu ya yaliyoteremshwa kwa mja Wetu, basi leteni sura moja mfano wake, na waiteni mashahidi wenu, mbali na Mwenyezi Mungu, ikiwa mnasema kweli." (Qur’ani 2:23)
Watu waliomkataa Mtume Muhammad (s.a.w) walishindwa katika ushindani huu, ingawa walikuwa na ufasaha mkubwa katika lugha ya Qur’ani tukufu. ushindano huu bado upo hadi leo.
Hakuna Migongano
Watu wanapoandik hawana budi kufanya makosa kama vile herufi, sarufi, taarifa zenye migongano, ukweli usio sahihi, na kughafilika na taarifa zingine.na makosa mingine mbalimbali
"Na kama ingekuwa kutoka kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, wangalipata ndani yake migongano mingi." (Qur’ani 4:82)
Qur’ani tukufu haina migongano yoyote – iwe ni katika maelezo ya kisayansi ya mzunguko wa maji, kiinitete, jiolojia na sayansi ya nyota; ukweli wa kihistoria na matukio; au utaabiri.
Je, Muhammad(S.A.W) Angeweza Kuiandika?
Mtume Muhammad (s.a.w) alijulikana kihistoria kuwa hakuwa na elimu; hakuweza kusoma wala kuandika. Hakuwa ameelimika katika uwanja wowote unaoweza kuelezea usahihi wa kisayansi na kihistoria, au uzuri wa kifasihi wa Kitabu hiki tukufu.
Usahihi wa simulizi za kihistoria za watu wa zamani na ustaarabu uliotajwa katika Qur’ani tukufu ni mkubwa sana kiasi kwamba hauwezi kuandikwa na mwanadamu yeyote.
"Wala Qur’ani hii haiwezi kuzushwa na yeyote asiyekuwa Mwenyezi Mungu." (Qur’ani 10:37)
Lengo la wahyi
Kuamini Mungu Mmoja wa Kweli
"Na Mungu wenu ni Mungu Mmoja. Hakuna mungu ila Yeye, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu." (Qur’ani 2:163)
Mada muhimu zaidi iliyotajwa katika Qur’ani ni imani kwa Mungu Mmoja wa Kweli.Mwenyezi Mungu anatufahamisha kwamba Hana mshirika, mwana, wala anayefanana naye, na hakuna anayestahili kuabudiwa isipokuwa Yeye peke yake.
Hakuna kinachoweza kufananishwa na Mwenyezi Mungu na hakuna kiumbe chake kinachofanana naye. Qur’ani pia inakataa wazo la kumhusisha Mwenyezi Mungu na sifa za mapungufu ya kibinadamu.
Kukataa Miungu Wote wa Uongo
"Muabuduni Mwenyezi Mungu wala msimshirikishe na chochote." (Qur’ani 4:36)
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu pekee ndiye anayestahili kuabudiwa,hivyo basi miungu ya batili na masanamu ya uongo lazima ikataliwe. Qur’ani tukufu pia inakataa wazo la kunasibisha sifa za kwa yoyote isipokuwa Mwenyezi Mungu.
Kusimulia Hadithi za Zamani
Qur’ani ina hadithi nyingi zenye mafunzo ya manufaa, zikiwemo hadithi za kweli za Manabii wa zamani kama vile Adam, Nuhu, Ibrahimu, Isa na Musa. Katika hadithi hizi, Mwenyezi Mungu anasema,
"Hakika katika hadithi zao mna mafunzo kwa wenye akili." (Qur’ani 12:111)
Kutukumbusha Siku ya Kiyama
Kitabu hiki Kitukufu kinatukumbusha kwamba watu wote watapitia mauti na watalipwa kwa matendo na maneno yao yote.
"Tutaviweka mizani za haki kwa ajili ya Siku ya Kiyama, ili nafsi yoyote isidhulumiwe hata kidogo..." (Qur’ani 21:47)
Kutimiza Njia Iliyokusudiwa ya Maisha
Muhimu, Qur’ani inatufundisha kwamba lengo la maisha ni kumwabudu Mwenyezi Mungu pekee, na kuishi maisha kwa mujibu wa njia aliyoiwekaMwenyezi Mungu.
Katika Uislamu, ibada ni dhana pana linalojumuisha matendo na maneno yote (ya siri au ya hadharani) ambayo Mwenyezi Mungu anayapenda na kuyakubali.
Kwa hivyo, kwa kutekeleza yale anayoyaamuru Mwenyezi Mungu, Muislamu anamuabudu Mungu na kutimiza lengo lake la maisha. Hizi ni mifano ya ibada yaliyopo katika Qur'an:
Kusali:
"Enyi mlioamini! Pigeni magoti na msujuduni, na mwabuduni Mola wenu ili mpate kufanikiwa." (Qur’ani 22:77)
Kutoa Sadaka:
"...Na toeni, bora kwa nafsi zenu; na wanaojiepusha na ubahili wa nafsi zao, hao hao ndio waliofanikiwa." (Qur’ani 64:16)
Kuwa Mkweli:
"Msichanganye haki na batili, wala msifiche kweli mkiwa mnaijua." (Qur’ani 2:42)
Kuwa na haya:
"Waambie Waumini wanaume wainamishe macho yao na wazilinde tupu zao... Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao na wazilinde tupu zao..." (Qur’ani 24:30-31)
Kuwa na Shukrani:
"Na Mwenyezi Mungu amewatoeeni kutoka matumboni mwa mama zenu huku mkiwa hamjui chochote, na amekujaalieni kusikia na kuona na nyoyo, ili mpate kushukuru." (Qur’ani 16:78)
Kuwa na uaadilifu:
"Enyi mlioamini! Simameni imara kwa ajili ya haki, kama mashahidi mbele ya Mwenyezi Mungu, hata ikiwa ni dhidi ya nafsi zenu, au wazazi wenu, au jamaa zenu, na ikiwa ni tajiri au maskini..." (Qur’ani 4:135)
Kuwa na Subira:
"Na vumilia, hakika Mwenyezi Mungu hapotezi thawabu za wanaofanya mema." (Qur’ani 11:115)
Kufanya Mema:
"Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walioamini na wanaotenda mema kwamba watapata msamaha na malipo makubwa." (Qur’ani 5:9)
Hitimisho:
Kwa muhtasari, Qur'ani inawafundisha wanadamu jinsi ya kumwabudu Mwenyezi Mungu Mmoja wa Kweli, na kwa hivyo kutimiza kusudi lao halisi la maisha, na kufanikisha mafanikio katika dunia na akhera.
"Hakika, tumekuletea wewe (Ewe Muhammad) Kitabu kwa ukweli kwa ajili ya wanadamu. Basi, yeyote anayekubali mwongozo, ni kwa faida yake mwenyewe; na yeyote anayepotea, anapotea kwa hasara yake mwenyewe."
Je, hujiwajibishi mwenyewe angalau kusoma Kitabu hiki Kitukufu?
